Friday, May 10, 2019

Mdude Chadema: Mwanasiasa wa Tanzania asimulia kisa cha utekaji wake na mateso aliyopitia


Mwanaharakati wa Tanzania Mdude NyagaliHaki miliki ya pichaMDUDE NYAGALI/ FACEBOOK

Mwanaharakati wa chama cha upinzani nchini Tanzania Mdude Nyagali ameelezea matuko yaliopelekea hadi kutekwa kwake kwa siku tatu kabla ya kujipata porini katika eneo la Mbeya.
Mdude ambaye aliokolewa na wanakijiji ambao walimpeleka katika hospitali ya eneo hilo alipatikana akiwa mchovu na aliyeteswa wakati wa kipindi chote cha utekaji wake.
Akizungumza na runinga ya MWANGItv nchini Tanzania katika kitanda chake hospitalini ambapo amelazwa, mwanaharakati huyo alisumilia kwamba watu waliomteka waliwasili na gari moja siku ya Jumamosi jioni nje ya makaazi yake.
Polisi wanachunguza tukio hilo na wamekanusha madai ya kuhusika na kutekwa kwake



Mwanaharakati wa Tanzania Mdude Nyagali


Kulingana na mwanaharakati huyo ambaye wakati wote huo alikuwa akiwaangalia watu hao kupitia dirisha la kibanda, cha kushangaza ni kwamba waliokua ndani ya gari hilo walisalia ndani bila kutoka.
''Ilipofika kati ya saa kumi na moja na kumi na mbili jioni watu hao walikuja hadi pale nilipokuwa na kuanza kuomba vocha ya simu wakati mimi nilikuwa katika mtandao ndani ya simu yangu. Nikawaambia sina akarudi ndani ya gari alilokuwemo''.
Mwanaharakati huyo anaelezea kwamba alianza kuwa na wasiwasi akaamua kurudi nyumbani kwake.
Anasema kwamba wakati huo alikuwa amebaba stakabadhi muhimu, ikiwemo simu na laptopu yake.
Anaongezea kwamba alipokuwa akielekea nyumbani kwake watu watatu walitoka ndani ya lile gari na kumfuata hadi karibu na mlango wa nyumba yake.
Anasema kwamba mmoja ya watu hao alisimama upande wake wa kushoto mwengine upande wa kulia na watatu akasimama katikati.
''Mimi niliegemea ukuta mmoja akaniambia ndugu sisi ni askari tunahitaji kuondoka nawe, nikawauliza wajitambulishe'', alisema
Lakini jamaa hao watatu walianza kumkaribia na alivyoona vitendo vyao akaanza kurudi nyuma akijaribu kutoroka lakini mmoja akamwambia mwenzake aliyekuwa karibu naye ''kamata begi na simu ndio vitu muhimu''
Mwanaharakati huyo ambaye alionekana kuwa na maumivi akisumilia kisa hicho anasema kuwa alijaribu kutoroka na begi hilo lakini mmoja ya watekaji hao alilikamata begi lake na kuanza kuvutana nalo

Nilivuta begi langu nikaona hataki kuachilia nami nikaanza kupiga kelele ili watu wakusanyike mahala nilipokuwa kwa sababu tayari giza lilikuwa limeanza kuingia''.
Anasema aliimarisha kelele zake kwa kuwa eneo analoishi ni karibu na kituo kimoja cha polisi na mita kumi kutoka kwa benki.
Anasema kwamba alipokuwa akipiga kelele za usaidizi jamaa hao walijaribu kumfunika mdomo na kufanikiwa kumnyang'anya begi lake lililokuwa na laptopu.
Walimburuta wakimuelekeza katika gari lao na watu walipojaribu kutaka kuingilia na kumsaidia mmoja wa watekaji hao anadaiwa kutoa bunduki na kuwatishia.
''Waliwatishia watu waliokuwa wamewasili kwa bunduki wakarudi nyuma, nami nilipoona vile nikaona hapa sasa ni kutetea nafsi yangu na nikaanza kupambana nao'', alisema Mdude.
Hatahivyo kulingana na mwanachama huyo wa chama cha upinzani nchini Tanzania Chadema, watu hao walimshinda nguvu na kumuingiza katika gari lao na kuondoka naye.
Awali baada ya taarifa za kutekwa Mdude kusambaa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, George Kyando alikanusha katika mahojiano yake na Gazeti la Mwananchi nchini Tanzania kusikika kwa milio ya risasi, siku iliotajwa.
"Mimi ni mkazi wa eneo linalodaiwa kuwa risasi zimepigwa lakini sijasikia na kama unavyojua mji wa Vwawa ni mdogo ambao zikipigwa risasi lazima utasikia," alisema.
Kamanda Kyando aliahidi kwamba ataendelea kufuatilia kwa kina taarifa hizo.
''Nikiwa ndani ya gari lile nilipigwa sana kwa kutumia chupa , walivua viatu nilivyokuwa nimevaa wakanipiga navyo usoni na masikioni na baadaye kunifunga kamba usoni na mdomoni na nikapoteza fahamu'', aliongezea Mdude.
Anasema kwamba alipopata fahamu alijipata katika msitu akiwa hajui aliko
Anaongezea kwamba alijaribu kutoa kamba ambazo alikuwa amefungwa mdomoni na kuanza kutafuta usaidizi
''Niliinuka nikaanza kutembea pole pole nikitafuta usaidizi hadi nikafika barabarani, nikiwa barabarani nilijaribu kusimamisha magari yaliokuwa yakipita lakini hayakusimama kwa zaidi ya saa moja hadi msamaria mwema mmoja aliposimama na kuwaita watu wa eneo la kijiji ili wanisaidie'', alisema
''Maneno niliyokuwa nikiyasikia masikioni mwangu ni mpige hivi mpige vile'', aliongezea .
Anasema kwamba kutekwa kwake kunahusiana na maswala ya kisiasa na ndio maana watekaji wake walichukua simu yake na laptopu.
''Simu na laptopu yangu zilikuwa na vitu muhimu sana , maswala ya chama, mambo ya kesi na mafunzo'', alisema
Hatahivyo mwanasiasa huyo amesisitiza kuwa hatosita kupigania haki za raia mbali na kuisahihisha serikali inapokosa na kuipongeza inapofanya vyema.
''Nitasimamia kupigania haki za watu , siwezi kunyamazia makosa. Tukiamua sote tuwe upande mmoja, viongozi wa chama tawala watakuwa na kazi gani?', aliuliza.
''Wana kazi kwa sababu kuna upinzani wakinipoteza mimi na wengine wengine watajitokeza na kuendelea'', alimaliza





No comments:

Post a Comment